×

Dk Mpango Aikabidhi ALAF Tuzo ya PMAYA na Uwekezaji Katika Ubora

Uongozi wa kampuni ya ALAF Limited umesema kuwa mafanikio yake ya hivi majuzi katika Tuzo za Rais za mzalishaji Bora wa Mwaka (PMAYA) umetokana na pamoja na mambo mengine uthabiti na uwekezaji mkubwa katika ubora uliofanywa na kampuni hiyo.

Akiogelea mafanikio hayo Meneja Uhusiano na Mawasiliano, Hawa Bayumi amesema kuwa uwekezaji bora umeiwezesha kampuni hiyo kushinda tuzo za PMAYA kwa mwaka wa 18 mfululizo.

Alisema kuwa, mwaka huu, kampuni hiyo imefanikiwa kupokea tuzo tatu kuu ambazo alisema ni pamoja na muonyeshaji bora katika maonyesho ya TIMExpo2024, Mshindi katika sekta ya uzalishaji wa bidhaa katika sekta ya uzalishaji chuma hiyo ikiwa ni mara ya 15 mfululizo na mshindi wa pili katika kitengo za mzalishaji bora wa mwaka wa 2024.

Mgeni rasmi katika hafla ya PMAYA mwaka huu, alikuwa ni Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango ambaye, aliongozana na viongozi wengine wa Serikali na Uongozi wa juu wa shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), ambao ndio waandaaji wakuu wa Tuzo hizo, ambazo zilifanyika hivi karibuni kwenye Ukumbi wa Superdome, Masaki jijini Dar es Salaam.

Alisema Tuzo hizo zinatambua kazi nzuri zinazofanywa na wazalishaji mbalimbali nchini Tanzania jmabo ambalo alisema linatoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.

“Malengo ya tuzo hizo ni matatu: kutambua ubora katika viwanda, kuhimiza ubunifu na kukuza ushirikishwaji, ambapo swala hili hushirikisha wazalishaji wote walioko hapa nchini”, alibainisha.

Aidha alisema ALAF ambayo ni kampuni kongwe hapa nchini, itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inaendelea kuwa kinara katika kukuza sekta ya ujenzi hapa nchini ili wananchi wapate bidhaa bora ambazo zinaakisi thamani ya fedha wanazotoa wakati wa kununua bidhaa za ujenzi yakiwemo mabati ya kuezekea.

“Katika kuweka msisitizo wa dhamira yetu hiyo, kiwanda chetu cha mabati ya rangi kiko tayari na kinatarajiwa kuanza uzalishaji Desemba, mwaka huu; hii ina maana hakutakuwa na haja ya kuagiza mabati yenye rangi nje ya nchi”, alisema.

Kwa mujibu wa Hawa, wahandisi vijana 30 tayari wamepitia mafunzo ya namna ya kuendesha mtambo huo wa kutengenezea mabati ya rangi na kwamba mtambo huo utaendeshwa na wafanyakazi wa wa Kitanzania kwa asilimia 100.

Aliushukuru uongozi wa CTI kwa mchango mkubwa kwa kampuni ya ALAF ambao alisema hauna kikomo, ambapo pia aliupongeza uongozi huo kwa kuandaa tuzo hizo ambazo alisema zinawahamasisha wazalishaji kuzalisha bidhaa zilizo bora hapa nchini.

Kampuni ya ALAF Limited (ALAF) ni kampuni inayoongoza kwa utengenezaji wa mabati ya kuezekea pamoja na bidhaa zingine za chuma hapa nchini, ambayo ilianzishwa mwaka wa 1960.

Kampuni hiyo imeendelea kuwa taasisi muhimu ya uwekezaji ambayo inatoa mchango mkubwa sana katika kukuza sekta ya ujenzi hapa nchini.

Kampuni ya ALAF imejikita kikamilifu katika uzalishaji, ambapo mbali na kuzalisha mabati ya kuezekea nyumba, pia inazalisha chuma aina mbalimbali pamoja na mabomba aina mbalimbali kwa ajili ya sekta ya ujenzi na matumizi mengine.

Leave a Comment