×

Balozi Charlotta Marcias: Mtaala Mpya utafanya wahitimu kuwa na ushindani Duniani

Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Marcias

Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Marcias ameiomba Serikali ya Tanzania kuendelea kufanya maboresho ya elimu hususani mitaala ili kuhakikisha wanafunzi wanaopitia katika Mfumo huo wanakuwa wavumbuzi, wataalam wabobezi na Viongozi wa Taifa lijalo.

Mhe. Marcias ameyasema hayo tarehe 21 Novemba, 2024 Manispaa ya Musoma mkoani Mara wakati wa ziara yake ya kujionea maendeleo ya miradi ya GPE LANES II na Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) inayofadhiliwa na baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya zikiwemo Sweden na Uingereza.

“nahimiza Serikali ya Tanzania kutenga walau asilimia 20 ya bajeti ya Taifa kwenye elimu ili kusaidia kufanya maboresho muhimu hususani mtaala. Kwa kuelimisha watoto wa leo, tutakuwa tunatengeneza nguvu kazi ya kesho ambayo itasaidia ukuaji wa uchumi, maendeleo ya kijamii na ushindani Duniani” alisema Mhe. Marcias.

Akitoa neno kabla ya kumkaribisha balozi huyo Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Kanali Evans Mtambi alisema Mkoa wa Mara unafarijika kuwapokea wageni hao kwani wamekuja kujionea msaada waliowapatia watu wa Mkoa wa Mara lakini amewahakikishia Wadau hao kuwa wamekuwa wanatumia fedha zinazotolewa zinatumika kama ilivyopangwa na wataendelea kufanya hivyo kulinda thamani ya fedha.

Balozi Charlotta Marcias ametembelea Kituo cha Walimu (TRC) Mwembeni Kata ya Mwigobero kilichokarabatiwa na kuwekwa samani kwa shilingi 22,000,000 kwa fedha za GPE LANES II na kupatiwa vifaa mbalimbali vya TEHAMA pia alitembelea shule ya sekondari ya ufundi Musoma iliyopatiwa shilingi 75,000,000 ambazo zilitumika kujenga madarasa mawili na kuweka samani.

Naye Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Elimumsingi ofisi ya Rais TAMISEMI, Suzan Nussu ambaye amemwakilisha Naibu Katibu Mkuu (ELIMU) Atupele Mwambene amewashukuru Wafadhili hao kwa kuendelea kujitoa katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha elimu nchini hususani miradi ya GPE LANES II na Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R).

MAZIKO ya NEEMA wa KARIAKOO ALIYEFARIKI AJALI ya GHOROFA KUPOROMOKA DAR…

Leave a Comment