
-Wajadili hali ya usalama katika Soko la Kariakoo.
-Aeleza dhamira ya Mkoa kuwa na mpangilio mzuri wa wafanyabiashara katika eneo la Kariakoo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amekutana na wadau mbalimbali wa Biashara katika eneo la Kariakoo pamoja na taasisi mbalimbali ikiwemo TANESCO, TANROAD, LATRA, DAWASA, Taasisi za fedha na Kamati ya Usalama ya Mkoa
Pamoja na mambo mengine kikao hicho kimejadili maswala mbalimbali yenye lengo la kuboresha ufanyaji biashara Kariakoo unaokidhi viwango vya kimataifa hususani hali ya usalama ambayo itawezesha biashara kufanyika saa 24, ambapo RC Chalamila ameipongeza Halmashauri ya Jiji kwa kuanza mchakato wa ununuzi wa Camera ambazo zinatarajiwa kufungwa maeneo mbalimbali ya mitaa ya Kariakoo.
Aidha Katika kupunguza msongamano kwenye eneo la kariakoo RC Chalamila amesema kupitia kikao hicho wamejadili mpango maalum shirikishi wa kuzuia aina zote za magari,bajaji na pikipiki kuingia katikati ya mitaa ya soko la kariakoo wakati wa asubui, mchana na jioni.
Vilevile RC Chalamila amesema eneo la kariakoo ni muhimu kibiashara linahudumia Tanzania na nchi jirani hivyo magari yataruhusiwa kuingia nyakati za usiku pekee ili kupunguza msongamano na kuruhusu biashara kufanyika bila usumbufu asubuhi hadi jioni