
MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka Watanzania kuwa wavumilivu na watulivu kuhusiana na suala la mauaji (kifo) ya Mzee Ali Kibao wakati vyombo vya ulinzi vikiendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.
“Kwanza nikiri kwamba waliofanya kitendo (mauaji) kwa ndugu yetu Ali Kibao, kitendo kile kilikuwa ni cha kihalifu sana. Hakuna mtu ambaye ataungana na wahalifu katika jambo hili. Sikutaka kulisema hili kwa undani kwa sababu ni moja ya matukio yaliyoleta hisia kwa umma, na moja ya matukio ambayo vyombo vyetu vya dola viko makini nayo katika kuhakikisha wanapata mnyororo wote wa watu ambao walifanya tukio hilo…Kwa hiyo niombe waandishi wa habari pamoja na Watanzania tuendelee kuwa na subira wakati vyombo vyetu vya dola vikikamilisha masuala ya kiuchunguzi,” amesema Chalamila.
RC Chalamila amayasema hayo leo tarehe 23 Desemba, 2024 katika mkutano na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Johari Rotana iliyopo jijini Dar es Salaam.