×

Watuhumiwa Wa Mauaji Ya Mtoto Greyson Aliyeuawa Kikatili Dodoma Wafikishwa Mahakamani

Watu wawili wamefikishwa mahakamani leo, Desemba 30, 2024, wakituhumiwa kwa shtaka la mauaji ya kukusudia ya mtoto Greyson Kanyenye (6). Mauaji hayo yanadaiwa kutokea Desemba 25, 2024, katika mtaa wa Ilazo, Kata ya Ipagala, jijini Dodoma.

Washtakiwa hao ni Kelvin Joshua (27), dereva wa bodaboda, na Tumaini Msangi (28), ambaye ni bondia. Wote wawili ni wakazi wa Ipagala, Dodoma.

Kesi hiyo imewasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma mbele ya Hakimu Mkazi Denis Mpelembwa. Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Patricia Mkina, alisema kuwa washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia kinyume na vifungu vya sheria namba 196 na 197 vya Kanuni za Adhabu.

Hakimu Mpelembwa alibainisha kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji, hivyo washtakiwa wamesomewa mashtaka yao bila kupewa nafasi ya kujibu lolote.

“Kosa la mauaji halina dhamana. Kwa sababu hiyo, mtarudi mahabusu hadi Januari 13, 2025, ambapo kesi yenu itatajwa tena,” alisema Hakimu Mpelembwa.

Leave a Comment