
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Desemba 30, 2024 amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mazishi ya Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko ambaye alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Akitoa Salama pole kwa waombolezaji nyumbani kwa marehemu Kondoa, Mkoani Dodoma, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameguswa na kifo cha Mheshimiwa Mwanaisha kwani alikuwa ni moja ya majaji wa mahakama ya rufani wenye uwezo mkubwa katika nafasi zote alizozitumikia.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Marehemu Mheshimiwa Mwanaisha alikuwa kiongozi aliyetekeleza wajibu wake kwa weledi na uadilifu “Msiba huu kwetu ni mzito, jukumu letu Wanakondoa, Watanzania, Majaji na wajumbe wa Tume ni kuendelea kumuombea kwa Mwenyezi Mungu”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa kila mmoja kuenzi yote mazuri aliyoyafanya Mheshimiwa Mwanaisha katika kipindi chake chote cha utumishi wa umma kwani kufanya hivyo kutakuwa ni njia nzuri ya kuweka kumbukumbu ya kazi zake.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma amesema kuwa Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko aliishi kiapo cha Uhakimu kwa kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo kutatua migogoro kwa uadilifu bila upendeo wowote,
“Mheshimiwa Mwanaisha alikuwa na ubinadamu na utu, maisha yake yalikuwa ni yakusaidia watu wengine, sisi tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwani uhai wake umetusaidia sana katika shughuli mbalimbali za kimahakama”