
Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Pamela Massaiy, Januari 2, 2025, amechukua fomu ya kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake wa Chadema Taifa (BAWACHA).
Pamela amesema lengo lake ni kuwaunganisha wanawake ndani ya chama na kuimarisha mshikamano wao. Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Pamela, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Afrika Mashariki kupitia CHADEMA na kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama, alisema ameamua kugombea nafasi hiyo kutokana na changamoto alizoziona ndani ya baraza hilo, ikiwemo kusuasua kwa utekelezaji wa maendeleo ya wanawake na kuwepo kwa rushwa.
“Nataka kuleta mabadiliko na kuhakikisha BAWACHA inakuwa chombo cha nguvu kinachowaunganisha wanawake na kuwa chachu ya maendeleo yao ndani ya chama… kama mnavyoelewa baraza letu linaongozwa kwa rushwa,” alisema Pamela.
Kwa sasa, nafasi hiyo ya Katibu Mkuu wa BAWACHA Taifa inashikiliwa na Catherine Ruge, ambaye pia amechukua fomu ya kutetea nafasi hiyo siku chache zilizopita.
Stori Na Elvan Stambuli.