Chester Griffiths (62), daktari wa ubongo anayeishi Malibu, Los Angeles nchini Marekani amegeuka shujaa katika janga la moto kwa kuonesha uwezo wa aina yake wa kupambana na moto kwa siku tano mfululizo.
Inaelezwa kuwa, Griffiths alikuwa ametoka kumaliza kufanya upasuaji ambapo aliondoka kwenye hospitali anayofanyia kazi na kurudi nyumbani kwake ambapo ghafla, moto mkubwa ulianza kuwaka.
Ilibidi aweke pembeni taaluma yake ya udaktari bingwa, akageukia fani ya zimamoto ambapo kwa kushirikiana na majirani zake wawili, walianza kupambana na moto huo kuzuia nyumba zao zisiteketee kwa moto.
Kuanzia siku hiyo, Griffiths na wenzake waliendelea na mapambano usiku na mchana na kufanikiwa kuokoa nyumba sita zisiguswe kabisa na moto.
“Kuna muda nilianza kufungasha mimi na familia yangu ili tuokoe maisha yetu kwa kuondoka lakini akili nyingine ikaniambia natakiwa kupambana kuokoa nyumba yangu na za majirani zangu, uzuri Griffiths akawa amefika, tukaanza kusaidiana,” Clayton Colbert, jirani wa Griffiths alinukuliwa na Gazeti la The Telegraph.