
Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limekuwa likishiriki mazoezi mbalimbali ya kijeshi ya pamoja baina yake na majeshi mengine ya nchi rafiki duniani.
Katika ushiriki wetu JWTZ kwa sasa linaendelea na maandalizi ya mazoezi mawili ya kijeshi yatakayofanyika hapa nchini yanayojulikana kama ‘Justified Accord’ na ‘Cutlass Express’ yatakayoshirikisha Jeshi la Marekani na Majeshi mengine kutoka nchi kumi na mbili.
Zoezi la Kijeshi la Justified Accord ni zoezi la nchi kavu linalotarajiwa kufanyika eneo la Msata Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani na Nanyuki nchini Kenya kuanzia Februari 10 mwaka huu kwa ushirikiano wa Tanzania na Marekani.
Zoezi hili litazinduliwa rasmi Februari 10 mwaka huu na linatarajiwa kufungwa Februari 21 mwaka huu.
Kufanyika kwa zoezi hilo kutatoa fursa kwa vikundi shiriki kuongeza weledi na uelewa wa pamoja wa kupambana na matishio mbalimbali ya kiusalama kama vile ya ugaidi.
Zoezi lingine la ‘Cutlass Express’ ni zoezi litakalofanyika kwa ajili ya kujenga uelewa wa pamoja na ushirikiano katika kukabiliana na matishio ya ulinzi na usalama katika maeneo yetu ya uwajibikaji baharini ikiwa ni pamoja na kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya.
Zoezi hilo na la Jeshi la Wanamaji linalotarajiwa kufanyika katika nchi za Tanzania, Madagascar na Ushelisheli kuanzia Februari 10 mwaka huu na kufungwa Februari 21 mwaka huu ambapo kwa Tanzania litafanyika katika jiji la Tanga.
Zoezi hilo litashirikisha nchi 14 ikiwemo Marekani ambayo inashirikiana na Jeshi la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika maandalizi ya majeshi hayo hapa nchini.
Nchi waalikwa katika zoezi hilo ni pamoja na Kenya, Madagascar, Ushelisheli, Djibout, Comoro, Georgia, Msumbiji, Malawi, Mauritius, Tunisia, Somalia na Senegal.
Katika mazoezi hayo imeelezwa kuwa inatarajiwa kuwepo kwa ongezeko la matumizi ya ndege vita, meli vita hivyo wananchi wametakiwa kutokuwa na taharuki.