
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, amezidi kutilia mkazo juu ya mfumo wa ugawaji wa majimbo ya uchaguzi nchini, akidai kuwa umejaa upendeleo mkubwa na unaminya uwakilishi wa kidemokrasia, hasa kwa vyama vya upinzani.
Akizungumza mkoani Dar es Salaam, Machi 2, 2025 katika mkutano kati ya CHADEMA na Jukwaa la Wahariri (TEF) uliofanyika Makao Makuu ya chama hicho, Lissu amesema kuwa majimbo 264 ya sasa yamegawanywa kwa upendeleo mkubwa katika ngazi mbalimbali.
“Majimbo haya yametengenezwa kwa upendeleo mkubwa sana – upendeleo kati ya Tanganyika na Zanzibar, kati ya miji na vijijini, na kati ya mikoa na mikoa. Matokeo yake, dhana ya usawa wa uwakilishi wa umma imevurugwa kabisa,” amesema Lissu.
Kwa mujibu wa Katiba, majimbo yanapaswa kugawanywa kwa kuzingatia vigezo viwili: uwepo wa miundombinu kama barabara, umeme, na reli; na hali ya kijiografia kama vile ukubwa wa eneo, milima, mabonde, na misitu. Hata hivyo, Lissu amehoji uhalali wa vigezo hivi kwa sababu havizingatii idadi ya watu wanaowakilishwa.
“Jiulize, haya majimbo ni kwa ajili ya uchaguzi wa binadamu au kwa ajili ya kuangalia wapi tutaweka barabara na umeme? Kwa nini idadi ya watu haizingatiwi?” amehoji Lissu.
Ameeleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, katiba ya Tanzania ilikuwa ikitumia kigezo cha idadi sawa ya watu katika kugawa majimbo, kama ilivyokuwa kwenye Katiba ya Uhuru ya 1961, Katiba ya Jamhuri ya 1962, na hata Katiba ya Mpito ya 1965. Lakini baada ya mwaka 1992, mfumo huo uliondolewa na badala yake kigezo cha kijiografia kikapewa kipaumbele, hali inayoongeza upendeleo mkubwa wa kisiasa.
Akitoa mfano wa athari za mfumo huu, Lissu amesema: “Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Jimbo la Temeke lilikuwa na wapiga kura 478,000 waliomsimamisha mbunge mmoja. Lakini kwa upande wa Zanzibar, majimbo yote 50 yalikuwa na wapiga kura 566,000 tu, ambao waliwachagua wabunge 50. Hii ina maana kwamba mbunge mmoja wa Temeke anawakilisha watu wengi zaidi kuliko wabunge wote wa Zanzibar kwa pamoja, lakini bado wote wanalipwa mshahara sawa na posho sawa.”