
Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limetoa taarifa ya chanzo cha ajali ya Basi la kampuni ya Mvungi lililokuwa likitokea Ugweno kwenda jijini Dar es Salaam, lililopata ajali na kusababisha vifo vya watu saba.
Mmoja kati ya mashuhuda ameeleza kuwa dereva wa basi lililopata ajali alikuwa akikwepa moja kati ya magari yaliyokuwa kwenye msafara wa msiba.
Jeshi la polisi limeeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo iliyotokea katika Kijiji cha Mamba Msangeni, Kata ya Msangeni Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, ni uzembe wa dereva ambaye alishindwa kulimudu basi hilo wakati akipishana na gari dogo na kusababisha liache njia na kupinduka katika bonde.
Taarifa iliyotolewa Alhamisi, April 3, 2025 na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, imesema kuwa kati ya watu waliopoteza maisha, wanaume ni wawili na wanawake ni watano akiwemo mtoto wa miaka miwili huku majeruhi wakiwa 42.