×

Waziri Mkuu Majaliwa Awasilisha Bajeti Ya Ofisi Ya Waziri Mkuu Na Bunge – Video

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kwa kipindi cha Agosti Mosi 2024 mpaka Februari 2025, Jumla ya shilingi Bilioni 54.9 zimekusanywa kwenye huduma ya usafiri wa reli kati ya Dar Es salaam – Morogoro – Dodoma.

Waziri Mkuu Majaliwa amebainisha hayo leo Aprili 09, 2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akitoa hotuba yake ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa mwaka 2025/2026, akieleza pia kwamba katika kipindi hicho jumla ya abiria 1,809, 983 wamesafirishwa kupitia usafiri huo wa wa reli.

“Uwepo wa huduma hiyo ya treni, umepunguza muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma kutoka wastani wa saa 10 kwa basi hadi kati ya saa tatu na nne na kuchagiza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.” Amesema Waziri Mkuu.

Aidha Waziri Mkuu Majaliwa ameliambia Bunge kuwa serikali ya awamu ya sita inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa ambapo hadi kufikia Februari 2025 Ujenzi kipande cha kutoka Mwanza- Isaka (Km 341) umefikia asolimia 62.37, Makutupora-Tabora (Km 368) umefikia asilimia 14.53, Tabora- Isaka (Km 165)umefikia asilimia 6.33 na Tabora- Kigoma umefikia asilimia 7.3.

Mhe. Waziri Mkuu pia amesema maandalizi ya kuanza ujenzi wa kipande cha Uvinza- Malagarasi – Musongati (Km 282) yameshaanza ambapo serikali ua Tanzania na Burundi zimesaini Mkataba wa Ujenzi wa kipande hicho Januari 29, 2025.