
Treni ya kwanza ya mizigo ya reli ya kisasa ya kiwango cha kimataifa (SGR) imewasili leo mchana katika kituo cha Ihumwa, jijini Dodoma, ikitokea stesheni ya Pugu, Dar es Salaam.
Treni hiyo, ikiwa na mabehewa 10 na kubeba jumla ya tani takribani 700 za mizigo mbalimbali, imetimiza ahadi ya kuanza rasmi huduma ya usafirishaji mizigo kwa kutumia SGR.
Hatua hii inaweka historia kwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki kuanzisha huduma ya treni ya mizigo kupitia reli ya kiwango cha kimataifa – ikionesha mafanikio ya kimkakati katika sekta ya usafirishaji na miundombinu.
Huduma hii inalenga kuimarisha ufanisi wa usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kuelekea mikoa ya kati na hatimaye nchi jirani, hivyo kuongeza ushindani wa Tanzania katika biashara ya kikanda na kimataifa.
