×

Wananchi wa Buchosa Wamshukuru Rais Samia kwa Msaada wa Milioni 70 kwa Ujenzi wa Miundombinu

Wananchi wa Jimbo la Buchosa wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa shilingi milioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo katika Shule ya Msingi Nyashana, iliyopo Kata ya Kalebezo.

Shukrani hizo zimetolewa na Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo, wakati akikabidhi rasmi fedha hizo kwa uongozi wa shule hiyo, kwa lengo la kuboresha mazingira ya ujifunzaji na kufundishia.

“Wananchi wa Buchosa tunalo deni kwa Mama Samia ambalo tunapaswa kulilipa mwezi Oktoba kwa kumpigia kura ya ndiyo,” alisema Shigongo huku akiwataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuleta maendeleo vijijini.

Msaada wa Vivuko Kati ya Visiwa

Mbali na mchango wa uboreshaji wa miundombinu ya elimu, wananchi pia wamemshukuru Rais Samia kwa msaada wa vivuko vya maji vinavyowezesha usafiri kati ya visiwa vya Buchosa na maeneo ya bara.

Vivuko hivyo ni:

MV Mwanza, inayotoa huduma kati ya Nyakaliro na Kome,

MV Sengerema, inayofanya safari kati ya Kanyala, Kasalazi na visiwa vya Soswa.

Maboresho hayo yameelezwa kuwa yataongeza usalama wa abiria, kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii, na kuchochea maendeleo ya maeneo ya visiwani ndani ya Jimbo la Buchosa.