The House of Social Media
gunners X

Tume Ya Uchunguzi Yaanza Kazi: Jaji Chande Aeleza Mambo 6 Makuu Yatakayochunguzwa – Video

0
Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu Mstaafu Mohammed Chande Othman.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu Mstaafu Mohammed Chande Othman, leo Disemba 1, 2025, ametaja rasmi maeneo sita ambayo yatakuwa kiini cha kazi ya tume hiyo.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jaji Chande alisema tume hiyo imepewa mamlaka ya kuchunguza kwa kina kile kilichosababisha uvunjifu wa amani, madhara yaliyojitokeza na hatua zilizochukuliwa na mamlaka mbalimbali kabla na baada ya tukio hilo.

Alisema uchunguzi huo unalenga kutoa picha kamili ya kile kilichotokea, nani alihusika, na nini kifanyike ili taifa libaki salama na kuendeleza misingi ya utawala bora.

Mambo 6 Yatakayochunguzwa

1. Chanzo cha matukio ya uvunjifu wa amani
Tume itaanza kwa kuchunguza na kubaini chanzo halisi cha matukio yote yaliyotokea wakati wa uchaguzi na mara tu baada ya uchaguzi huo.

2. Lengo la wahusika
Itachunguza kwa undani lengo lililokusudiwa na makundi au watu waliopanga na kutekeleza vitendo hivyo, ikiwemo dhamira yao na malengo yao ya mwisho.

3. Madhara yaliyotokea
Tume itakusanya taarifa na ushahidi kuhusu vifo, majeruhi, uharibifu wa mali pamoja na athari za kiuchumi na kijamii zilizosababishwa na matukio hayo.

4. Hatua zilizochukuliwa na mamlaka
Uchunguzi pia utagusa hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali, vyombo vya usalama, na watu wengine waliokuwa na dhamana katika kipindi cha uchaguzi.

5. Mapendekezo ya kuimarisha mfumo wa uwajibikaji na amani
Tume itatoa mapendekezo kuhusu namna ya kuimarisha uwajibikaji wa viongozi na raia, kulinda amani, kutetea haki za binadamu, kuimarisha utawala wa sheria na kufikia maridhiano ya kitaifa.

6. Masuala mengine muhimu
Kwa mamlaka iliyonayo, tume itachunguza pia jambo lolote jingine litakaloonekana lina umuhimu na linaloendana na majukumu yake.

Jaji Chande alisisitiza kuwa kazi ya tume hiyo ni ya kitaifa na inalenga kuhakikisha ukweli unajulikana, changamoto zinatambuliwa, na njia bora za kuzuia matukio kama hayo zinatengenezwa kwa ajili ya mustakabali wa taifa.

Leave A Reply