Niffer Awashukuru Watanzania Baada ya Kuachiwa Huru – Video

Mfanyabiashara maarufu Jennifer Jovin, anayejulikana mtandaoni kama Niffer ameishukuru serikali na wananchi kwa mshikamano waliomuonyesha kipindi chote alichokuwa akishikiliwa hadi kuachiwa kwake leo, Desemba 3, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutoka gerezani, Jennifer amesema ameguswa na upendo alioupokea kutoka kwa Watanzania waliojitokeza kumuunga mkono yeye na familia yake katika kipindi kigumu.
“Nawashukuru sana Watanzania kwa kuwa karibu nami kwa kipindi chote nilichokuwa nikishikiliwa. Wengi mliweza kufika gerezani, mkatusaidia mimi na familia yangu kwa hali na mali. Upendo wenu siwezi kuusahau,” amesema.
Jennifer amesisitiza pia kuwa hana chama chochote cha siasa na hajawahi kujihusisha na shughuli za kisiasa.
“Sina chama chochote cha siasa, wala sijihusishi na siasa. Mimi ni Mtanzania kama wengine wote. Namshukuru sana mama yangu kwa jinsi alivyonipigania, na namshukuru Mheshimiwa Rais,” ameeleza.
Amshukuru Rais Samia kwa Msamaha
Jennifer ameonyesha shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuagiza kutolewa kwa msamaha kwa baadhi ya watu waliokuwa wakikabiliwa na mashitaka ambao kwa mujibu wake “walifuata mkumbo”.
“Nashukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake. Kimsingi wengi walikuwa wamenaswa kwa kufuata mkumbo. Uamuzi wake umeleta faraja kubwa sana,” amesema.
Ataka Watanzania Kuwatembelea Wafungwa na Kuepuka Vurugu
Aidha, Jennifer ametoa wito kwa Watanzania kuwatembelea watu wanaoshikiliwa gerezani ili kuwapa faraja, akisisitiza kuwa thamani ya uhuru ni kubwa kuliko wengi wanavyodhani.
“Uhuru una thamani kubwa sana. Amani ina thamani kubwa sana. Vurugu zinaumiza. Kuna watu waliokwama gerezani kwa sababu tu ya vurugu kutokea, kesi zao zimesimama. Ni vyema kila mmoja kujiepusha na vurugu,” amesema.
Jennifer amemalizia kwa kuomba Watanzania waendelee kuenzi upendo, amani na mshikamano ambao Tanzania imezoeleka nao kwa muda mrefu.

