Machado aapa kurudi Venezuela Amshukuru Trump na kutaka uchaguzi huru

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Venezuela, Maria Corina Machado, ameapa kurejea nyumbani “haraka iwezekanavyo” na kusisitiza kuwa nchi hiyo iko tayari kwenda kwenye uchaguzi huru na wa haki.
Machado, ambaye kwa sasa yuko uhamishoni, aliondoka Venezuela Oktoba mwaka jana akiwa mafichoni, kuelekea kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Fox News, alisema hatua iliyochukuliwa na Marekani dhidi ya rais wa zamani Nicolas Maduro imefungua ukurasa mpya wa matumaini kwa wananchi wa Venezuela.

“Napanga kurudi Venezuela haraka iwezekanavyo,” alisema Machado, wakili na mama wa watoto watatu.
Ameeleza kuwa uchaguzi wa mwaka 2024 ulifanyika katika mazingira magumu, lakini bado anaamini walishinda, akidai kuwa katika uchaguzi huru, upinzani unaweza kupata zaidi ya asilimia 90 ya kura.
Amshukuru Rais Donald Trump
Machado pia alimpongeza Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa hatua alizochukua dhidi ya adui yake wa kisiasa, Nicolas Maduro, na kusisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa ina wajibu wa kusaidia kuchangia amani na demokrasia nchini Venezuela.
Hata hivyo, amesema hajawasiliana moja kwa moja na Trump tangu alipokabidhiwa tuzo ya Nobel tarehe 10 Oktoba.
Anatafutwa na Serikali
Pamoja na kutangaza mpango wa kurejea nyumbani, Machado bado anatafutwa na serikali ya chama tawala. Licha ya hilo, amesema hatishiki, kwani anaamini wananchi wanahitaji mabadiliko ya kweli.
Kwa sasa, inaonekana Marekani inaweza kushirikiana na Rais wa mpito Delcy Rodriguez, mshirika wa karibu wa Maduro, ambaye amelaani tukio la kukamatwa kwa Maduro lakini pia ametoa wito wa kuendeleza mazungumzo na Washington.

