
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Reuben Kwagilwa (Mb), ametoa muda wa mwezi mmoja kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kuhakikisha unakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara katika Shule ya Sekondari Kiutu, ambao umeanza tangu mwaka 2024 bila kukamilika.
Kwagilwa ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya ukaguzi shuleni hapo, ambapo ameonesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo unaolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Amesema amesikitishwa na hali ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kiutu kusoma kwa kipindi cha miaka minne bila kuwa na maabara za sayansi, jambo linaloathiri ubora wa elimu, hasa kwa masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia yanayohitaji majaribio ya vitendo.
Aidha, Naibu Waziri huyo ameshangazwa na baadhi ya wanafunzi kulazimika kusomea katika chumba cha maktaba kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa, hali ambayo si rafiki kwa mazingira ya ujifunzaji na inaleta changamoto katika usimamizi wa taaluma shuleni hapo.

“Natoa mwezi mmoja watoto wasomee hapa msiendelee huku juu tena badala yake fedha zote zielekezwe kwenye maabara hii shule mwaka huu inakwenda kuwa na form four, Afisa mipango na mkurugenzi jitafakarini sana watoto wanaaza form one mpaka form four hawajawahi kuiona maabara sasa wanaenda kushindanaje na watoto wengine?,” amesema Mhe. Kwagilwa.
Shule ya Sekondari Kiutu ni miongoni mwa shule za sekondari za kata zilizojengwa kupitia mradi wa SEQUIP, unaotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuongeza fursa za elimu ya sekondari, kuboresha miundombinu na kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi nchini.