
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa niaba ya Wizara, Idara na Wakala za Serikali (MDAs) pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs), imetangaza nafasi 912 za ajira kwa Watanzania wenye sifa na uwezo, kufuatia tangazo lililotolewa Januari 14, 2026.
Kwa mujibu wa tangazo hilo lenye kumbukumbu namba JA.9/259/01/C/16, nafasi nyingi zimetengwa kwa kada ya ualimu, hususan masomo ya Sayansi, pamoja na nafasi chache za walezi wa watoto.
Tangazo linaeleza kuwa nafasi 709 ni za Mwalimu Daraja la III C – Hisabati, ambapo watakaoteuliwa watakuwa na majukumu ya kuandaa maandalio ya masomo, kufundisha, kufanya tathmini za wanafunzi, kusimamia mahudhurio, kutoa ushauri wa kitaaluma na kushiriki katika malezi ya wanafunzi kwa ujumla. Waombaji wanatakiwa kuwa na Shahada ya Elimu au Shahada ya Ualimu yenye somo la Hisabati, au Shahada isiyo ya Ualimu yenye somo la Hisabati pamoja na Stashahada ya Uzamili ya Elimu. Nafasi hizi zinalipwa kwa ngazi ya mshahara TGTS – D.
Aidha, nafasi 201 zimetengwa kwa Mwalimu Daraja la III C – Fizikia, wenye majukumu yanayofanana na ya walimu wa Hisabati, ikiwemo kufundisha, kutathmini wanafunzi na kusimamia maendeleo ya elimu shuleni. Sifa za waombaji ni kuwa na Shahada ya Elimu au Ualimu yenye somo la Fizikia, au Shahada isiyo ya Elimu pamoja na Stashahada ya Uzamili ya Elimu. Nafasi hizi pia zinalipwa kwa ngazi ya mshahara TGTS – D.
Vilevile, nafasi mbili (02) zimetengwa kwa Mlezi wa Watoto Msaidizi (Child Care Assistant), ambao watakuwa na majukumu ya kushiriki katika utekelezaji wa programu za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto, kuandaa ratiba za shughuli za kila siku, kutoa ushauri kwa wazazi na kushiriki katika uhamasishaji wa jamii kuhusu huduma za watoto. Waombaji wanatakiwa kuwa wahitimu wa Kidato cha Nne au Sita waliopata Astashahada ya Elimu ya Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto, Ustawi wa Jamii au Saikolojia kutoka vyuo vinavyotambuliwa na Serikali. Nafasi hizi zinalipwa kwa ngazi ya mshahara TGS B.
Tangazo hilo linafafanua kuwa waombaji wote wanapaswa kuwa raia wa Tanzania wasiozidi umri wa miaka 45, huku waombaji wenye ulemavu wakihimizwa kuomba na kuainisha hali zao kwenye mfumo wa maombi ya ajira. Waombaji wanatakiwa kuwasilisha vyeti vya kuzaliwa, elimu na taaluma vilivyothibitishwa kisheria, huku nyaraka za muda kama “provisional results” au “result slips” zikibainishwa kuwa hazitakubaliwa.
Kwa waombaji waliosoma nje ya Tanzania, wametakiwa kuhakikisha vyeti vyao vimethibitishwa na mamlaka husika ikiwemo TCU, NECTA na NACTVET. Aidha, waombaji waliostaafishwa katika Utumishi wa Umma hawaruhusiwi kuomba isipokuwa kama wana kibali cha Katibu Mkuu Kiongozi.
Mwisho wa kutuma maombi ya ajira ni tarehe 28 Januari, 2026, na maombi yote yanapaswa kuwasilishwa kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ajira (Recruitment Portal) wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

