Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amekutana na Wakuu wa Mikoa wapya  wa Mkoa wa Kagera na Mtwara, Mhe. Kanali Yahya Ramadhani Kido na Mhe. Kanali Donald Wiliam Msengi ili kujipanga kiutendaji katika kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa ili kuimarisha ufanisi na uwajibikaji katika kuwatumikia wananchi.

Prof. Shemdoe amekutana na Wakuu  hao leo Februari 09, 2026 katika Ofisi Ndogo ya TAMISEMI Jijini Dar es Salaam, mara baada ya viongozi hao kuapishwa na Mhe. Rais katika Ikulu ya Magogoni, ambapo Mhe. Rais amewataka viongozi hao kwenda kuimarisha uwajibikaji ili kukidhi matarajio ya wananchi hususani kwenye eneo la upatikanaji wa huduma za kijamii pamoja na ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao.