
Kiungo mshambuliaji wa Benfica, Gianluca Prestianni (20), amepewa adhabu ya kusimamishwa kwa muda mechi moja na UEFA kufuatia tuhuma za kutoa kauli ya kibaguzi dhidi ya Vinícius Júnior wa Real Madrid.
Tukio hilo lilitokea katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa play-off ya UEFA Champions League uliochezwa Lisbon wiki iliyopita. Vinícius alimuarifu mwamuzi Francois Letexier kuhusu kauli aliyodai kusikia, jambo lililosababisha mwamuzi kuanzisha itifaki ya UEFA dhidi ya ubaguzi, na mchezo kusimama kwa takriban dakika 10.
Prestianni amepewa adhabu ya kusimamishwa kwa muda mechi moja, hivyo hatakuwepo katika marudio dhidi ya Real Madrid siku ya kesho Saintiago Bernabeu.
Iwapo atapatikana na hatia, kanuni za UEFA zinaeleza anaweza kufungiwa angalau mechi 10. Prestianni amekanusha tuhuma hizo akidai hakutoa kauli ya kibaguzi na kwamba kulikuwa na kutokuelewana.
Benfica waliunga mkono mchezaji wao kwa kushiriki upya kauli yake wakisema: “Together, by your side.”
Real Madrid wataingia kwenye mechi hiyo marudiano wakiwa na uongozi wa 1-0 baada ya Vinícius kufunga bao pekee katika mchezo wa kwanza. Kocha wa Benfica, Jose Mourinho, naye atakosa mechi hiyo baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu Lisbon.