
Rais wa Marekani, Donald Trump, ameongeza muda wa kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Iran kwa siku 10 zaidi, hatua inayolenga kutoa nafasi kwa mazungumzo ya amani kuendelea.
Kwa mujibu wa tangazo lake, mashambulizi hayo sasa yamesogezwa hadi Aprili 6, 2026 saa 8 usiku (Eastern Time), hatua aliyosema imechukuliwa kufuatia ombi kutoka uongozi wa Iran huku akisisitiza kuwa mazungumzo yanaendelea vizuri.
Israel Yabadili Mkakati
Wakati Marekani ikisukuma diplomasia, Israel imeelekeza nguvu zake kwenye kushambulia viwanda vya silaha vya Iran ili kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa taifa hilo.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, anaonekana kubadili mwelekeo kwa muda, akipunguza msukumo wa wazi wa mabadiliko ya utawala (regime change) ndani ya Iran.
Jeshi la Israel (IDF) limeripotiwa kulenga:
- Vituo vya uzalishaji wa makombora na silaha za majini mjini Tehran
- Kiwanda cha vilipuzi katika mji wa Isfahan
Marekani Yadai Mafanikio ya Mashambulizi
US Central Command imesema mashambulizi ya pamoja tayari yameharibu kwa kiasi kikubwa miundombinu ya Iran inayotumika kutengeneza makombora, ndege zisizo na rubani (drones), na manowari.
Mchambuzi wa masuala ya Iran, Farzin Nadimi, amesema Israel inatumia fursa hii kupunguza uwezo wa kijeshi wa Iran kabla ya kusitisha operesheni.

Hali ya Biashara Duniani Yatetereka
Mvutano huu umeathiri vibaya biashara ya kimataifa, hasa baada ya Iran kuweka mabomu ya majini katika njia ya Strait of Hormuz, hatua iliyosababisha kupanda kwa bei za mafuta duniani.
Aidha, Iran imetishia kufunga njia nyingine muhimu ya biashara ya Bab al-Mandab Strait, inayounganisha Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden hatua inayoweza kuathiri usafirishaji kati ya Ulaya na Asia.
Hofu Yaongezeka
Licha ya mashambulizi hayo, baadhi ya maafisa wa zamani wa usalama wa Israel wana wasiwasi kuwa Iran bado haijaacha mpango wake wa nyuklia, ikiwemo:
- Uboreshaji wa uranium
- Hifadhi ya silaha
- Makombora ya masafa marefu
Wakati vita vikikaribia kutimiza mwezi mmoja, juhudi za kidiplomasia zinaendelea huku dunia ikifuatilia kwa karibu hatma ya mzozo huu ambao unaweza kuathiri uchumi wa dunia kwa kiwango kikubwa.