
Mbunge wa Jimbo la Makete kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Festo Sanga, ameuliza swali la nyongeza Bungeni akilenga Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Katika swali lake, Sanga amehoji mkakati wa Serikali katika kukamilisha ujenzi wa arena ya kisasa itakayosaidia kukuza sekta ya muziki, kwa kuwawezesha wasanii kufanya maonesho katika mazingira bora pamoja na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, amesema mchakato wa ujenzi upo katika hatua za mwisho, huku akibainisha kuwa ujenzi unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Ameongeza kuwa Serikali imetenga shilingi bilioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa arena hiyo pamoja na studio ya kisasa kwa ajili ya utayarishaji wa filamu.
Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya msanii wa muziki wa Bongo Flava, Diamond Platnumz, kuhoji kuchelewa kwa ujenzi wa arena, jambo lililozua mjadala mpana miongoni mwa wasanii, akiwemo Harmonize aliyemjibu hadharani.