×

Mkuu wa Majeshi wa Marekani Ajiuzulu Baada ya Shinikizo la Uongozi

Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi (Army Chief of Staff), Randy George.

Mkuu wa Majeshi Marekani, Randy George, ameacha wadhifa wake kufuatia taarifa kwamba Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth, alimtaka ajiuzulu mara moja.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Pentagon, George ambaye alikuwa akihudumu kama Mkuu wa 41 wa Majeshi ya Jeshi la Ardhi, atastaafu “mara moja” kutoka nafasi hiyo.

Msemaji wa Pentagon, Sean Parnell.

Msemaji wa Pentagon, Sean Parnell, alithibitisha hatua hiyo akisema jeshi linathamini mchango wake wa muda mrefu kwa taifa na kumtakia mafanikio katika maisha yake ya baada ya utumishi.

Kwa kawaida, Mkuu wa Majeshi huhudumu kwa kipindi cha miaka minne. George aliteuliwa mwaka 2023 baada ya kupendekezwa na Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden, na kuthibitishwa na Seneti, hatua ambayo ilimaanisha angeendelea kuhudumu hadi mwaka 2027.

Kabla ya kushika nafasi hiyo ya juu, George alihudumu kama msaidizi mkuu wa kijeshi kwa Waziri wa Ulinzi wa wakati huo, Lloyd Austin, kati ya mwaka 2021 na 2022. Katika maisha yake ya kijeshi yenye uzoefu wa muda mrefu, George ni mhitimu wa Chuo cha Kijeshi cha West Point na amewahi kushiriki katika migogoro mbalimbali ikiwemo vita vya Iraq na Afghanistan.

Hatua ya kuondoka kwake inakuja katika kipindi ambacho Pentagon imekuwa ikifanya mabadiliko ya uongozi, ambapo maafisa kadhaa wa ngazi za juu wameondolewa au kubadilishwa. Taarifa zinaeleza kuwa mabadiliko haya yanaweza kuashiria mkakati mpana wa kubadilisha uongozi ndani ya jeshi la Marekani.

Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth.

Kwa sasa, nafasi ya George inashikiliwa kwa muda na Makamu Mkuu wa Majeshi, Jenerali Christopher LaNeve, ambaye atakuwa kaimu Mkuu wa Jeshi la Ardhi hadi uteuzi mpya utakapofanyika.

Hadi sasa, haijawekwa wazi sababu rasmi za kuondoka kwa George, lakini hatua hiyo imeibua mjadala mpana kuhusu mwelekeo wa uongozi na mabadiliko ndani ya Pentagon.

Hegseth amekuwa na malalamiko ya muda mrefu kuhusu Jeshi pamoja na mivutano iliyopo katika masuala ya uongozi na usimamizi wa rasilimali watu.

Leave a Comment