×

Iran Yatoa Masharti Kabla ya Kurejea Mazungumzo ya Amani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei amesema kuwa nchi yake haitajiunga na mazungumzo ya kidiplomasia bila kuwepo kwa mazingira yenye msingi wa mantiki yatakayolinda maslahi ya taifa hilo.

Akizungumza kupitia vyombo vya habari vya Iran, Baghaei alieleza kuwa mgogoro unaoendelea kati ya Iran na Marekani pamoja na Israel uliilazimishwa Iran, na kwamba hatua zote zilizochukuliwa na Tehran zimekuwa ndani ya haki yake ya kujilinda dhidi ya kile alichokiita uchokozi wa kijeshi.

Kuhusu kutohudhuria kwa Iran katika duru ya pili ya mazungumzo ya amani yaliyopangwa kufanyika Islamabad, Baghaei alisema diplomasia ni chombo muhimu lakini hutumika pale tu kunapokuwa na mazingira sahihi ya kufanikisha maslahi ya taifa.

“Diplomasia ni nyenzo ya kulinda usalama na maslahi ya kitaifa, lakini tutaitumia pale tu tutakapojiridhisha kuwa kuna msingi wa mantiki wa kufanikisha malengo hayo,” alisema.

Aidha, alisisitiza kuwa Iran itaendelea kutumia kila fursa kuwawajibisha wale wanaodaiwa kuhusika na uchokozi huo, ikiwemo kudai haki na fidia kwa madhara yaliyotokana na mgogoro huo.

Kauli hiyo inaonesha msimamo mkali wa Iran wakati huu ambapo juhudi za kidiplomasia zinaendelea kufanywa ili kupunguza mvutano unaoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati.

Kwa sasa, bado haijafahamika ni lini Iran itarejea rasmi kwenye meza ya mazungumzo, huku wachambuzi wakisema hatua hiyo itategemea maendeleo ya kisiasa na kiusalama katika siku zijazo.

IRAN YAFANYA MAONESHO MAKUBWA ya KIJESHI – MAKOMBORA ya BALISTIKI YAONESHWA MITAANI -MAELFU WAVUTIWA

Leave a Comment