
Rais wa Marekani, Donald Trump, ameondolewa kwa haraka na maafisa wa Secret Service baada ya milio ya risasi kusikika wakati wa hafla ya White House Correspondents’ Dinner iliyokuwa ikiendelea mjini Washington, DC.
Tukio hilo la kutisha lilitokea ndani ya ukumbi wa Washington Hilton, ambapo wageni waalikwa, wakiwemo viongozi wakuu wa serikali na wanahabari, walikumbwa na taharuki kubwa huku wakijaribu kujinusuru kwa kujificha chini ya meza.
Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka vyombo vya usalama, mshukiwa ametambuliwa kama mwanaume mwenye umri wa miaka 31 kutoka California, ambaye alikamatwa mara moja baada ya tukio hilo. Inadaiwa alikuwa na silaha kadhaa ikiwemo bunduki, bastola pamoja na visu, na alivamia eneo la ukaguzi wa usalama kabla ya kuzuiwa na maafisa wa ulinzi.

Mashuhuda wa tukio hilo wanasema hali iligeuka ghafla kuwa ya hofu baada ya mtu mmoja kukimbia kwa kasi kuelekea eneo la ulinzi, hali iliyowalazimu maafisa wa Secret Service kuchukua hatua za haraka kwa kutumia silaha zao kumzuia mshukiwa huyo.
Katika tukio hilo, afisa mmoja wa usalama alijeruhiwa baada ya kushambuliwa, lakini alinusurika kutokana na kuvaa vazi maalum la kuzuia risasi. Afisa huyo anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini huku hali yake ikiripotiwa kuwa nzuri.

Rais Trump, ambaye alitarajiwa kutoa hotuba katika hafla hiyo, aliondolewa salama pamoja na viongozi wengine waliokuwepo, akiwemo Makamu wa Rais JD Vance, Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth, na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio.
Baada ya tukio hilo, Trump alitoa tamko akieleza kuwa afisa aliyejeruhiwa yuko katika hali nzuri, huku akimtaja mshukiwa huyo kama “mtu hatari” aliyekuwa akifanya shambulio peke yake (lone wolf). Aidha, alisisitiza kuwa vyombo vya usalama vilifanya kazi kwa haraka na ufanisi kuzuia madhara makubwa zaidi.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mshukiwa huyo alidaiwa kumlenga moja kwa moja Rais Trump, ingawa uchunguzi zaidi unaendelea kubaini chanzo na nia halisi ya shambulio hilo.

Mamlaka za usalama nchini Marekani, zikiwemo Federal Bureau of Investigation (FBI), zimeanzisha uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo ambalo limeibua maswali mapya kuhusu usalama wa viongozi katika hafla kubwa za kitaifa.
Hafla hiyo ya kila mwaka, ambayo huwakutanisha viongozi wa serikali, wanahabari na watu mashuhuri, ilisimamishwa kufuatia tukio hilo huku usalama ukiimarishwa katika maeneo muhimu ya jiji la Washington, DC.


