×

Watoto 4,200 Waishio Mitaani Kuunganishwa na Familia Zao Nchini

Zaidi ya watoto 4,200 wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika mikoa mitano nchini, ikiwemo Pwani na Arusha, wanatarajiwa kuondolewa mitaani na kuunganishwa tena na familia zao kupitia mradi mpya wa ulinzi wa watoto waishio na kufanya kazi mitaani.

Mradi huo wa.sh. Bilioni 6.3 umezinduliwa na Serikali Mkoani Pwani kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la SOS Children’s Villages huko Kibaha ambapo kwa Mkoa wa Pwani utatekelezwa katika Halmashauri tano za Kibaha Manispaa, Kibaha Vijijini, Mkuranga, Bagamoyo, na Chalinze.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Kusirye Ukio, ambaye alikuwa mgeni rasmi,amesema  katika robo ya mwaka iliyoishia Juni 2026, Mkoa wa Pwani ulirekodi watoto 36 waishio mitaani na kwamba mradi huo unatarajiwa kusaidia kupunguza tatizo hilo.

Dkt. Ukio ametoa wito kwa jamii na wazazi mkoani humo kuwajibika kikamilifu katika malezi ili kuzuia watoto kukimbilia mitaani, akisisitiza kuwa suluhu ya kudumu inaanza na kuimarishwa kwa ustawi wa familia zenyewe.

Awali Meneja wa Shirika la SOS Children’s Villages, Damas Damas, amebainisha kuwa lengo kuu la mradi ni kupunguza wimbi la watoto mitaani kwa kuwahifadhi kwenye makao salama au kwa walezi wa kuaminika, kuwapatia huduma za urekebishaji wa kisaikolojia, na hatimaye kuwarudisha kwenye familia zao.

“Tunajua kabisa kuwa mtaa hauzai mtoto. Watoto hawa wanatakiwa kupata ulinzi, usalama, na malezi bora katika ngazi ya familia,” amesisitiza Damas.

Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Pwani, Mratibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Eliudy Malesa, ameeleza kuwa maisha ya mitaani yanawaweka watoto katika mazingira hatarishi yanayowasababishia kufanyiwa ukatili mkubwa ikiwemo ubakaji, huku wakikosa haki zao za msingi kama elimu na afya.

Leave a Comment