
Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi ya Mwenyekiti wa Tundu Lissu ya kutaka kuunganishwa katika kesi ya mgawanyo wa mali inayowahusisha aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohamed, pamoja na wenzake.
Wengine katika kesi hiyo ni Ahmed Rashid Khamis na Maulidah Anna Komu (marehemu).
Akizungumza mahakamani hapo, Wakili wa CHADEMA, Rugemeleza Nshala, amesema mahakama imetoa uamuzi wa kukataa maombi ya Lissu ya kuunganishwa katika kesi namba 8323.
Ameeleza kuwa maombi hayo yalisikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga, ambaye awali alipanga kutoa uamuzi tarehe 25 Machi 2026, lakini baadaye ulisogezwa kutokana na faili kupelekwa Mahakama ya Rufaa.
Kwa mujibu wa uamuzi uliosomwa na Msajili wa Mahakama, imeelezwa kuwa Lissu alifungua maombi hayo kwa jina lake binafsi na si kwa nafasi ya uenyekiti wa chama, hivyo mahakama imeona hana maslahi ya moja kwa moja katika shauri hilo.
Aidha, kesi hiyo sasa haipo tena kwa Jaji Hamidu Mwanga, bali ipo mbele ya Jaji Ngunyale, na imepangwa kutajwa tena Mei 13, 2026 kwa ajili ya maagizo, ikiwemo kujadili iwapo kesi ilifunguliwa ndani ya muda wa kisheria wa miaka sita tangu mgogoro kuanza.