×

Marekani Yaondoa Wanajeshi 5,000 Ujerumani Baada ya Mvutano wa Kidiplomasia

Serikali ya Marekani imetangaza mpango wa kuondoa takribani wanajeshi 5,000 walioko nchini Ujerumani, hatua ambayo inatajwa kuibua mjadala mpya kuhusu mustakabali wa uhusiano wa kijeshi kati ya Washington na washirika wake wa Ulaya.

Kwa mujibu wa taarifa ya Pentagon iliyotolewa Ijumaa, uondoaji huo unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 6 hadi 12 ijayo. Uamuzi huo unakuja wakati mvutano wa kidiplomasia ukizidi kuongezeka kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na baadhi ya viongozi wa Ulaya.

Ripoti zinaeleza kuwa uamuzi huo umechochewa na kauli na misimamo ya hivi karibuni kutoka kwa pande zote mbili, ikiwemo malumbano kati ya Trump na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, ambaye alikosoa namna Marekani inavyoshughulikia mzozo unaohusishwa na Iran.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Pentagon, ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema baadhi ya kauli kutoka upande wa Ujerumani zimekuwa hazisaidii na zinaathiri ushirikiano wa kimkakati.

Marekani imesema kuwa hatua hiyo inalenga kurudisha idadi ya wanajeshi wa Marekani barani Ulaya katika kiwango kilichokuwepo kabla ya mwaka 2022, kabla ya kuongezeka kwa vikosi kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Aidha, hatua hiyo inaonekana pia kuendana na msimamo wa utawala wa Trump wa kuhimiza mataifa ya Ulaya kuchukua jukumu kubwa zaidi katika ulinzi wa bara lao, badala ya kutegemea sana Marekani.

Uamuzi huu unatazamwa kama kipimo kipya cha uimara wa ushirikiano ndani ya muungano wa NATO, hasa katika kipindi ambacho masuala ya usalama wa Ulaya yanaendelea kuwa tete kutokana na migogoro ya kikanda.

Kwa sasa, hakuna taarifa rasmi kutoka serikali ya Ujerumani kuhusu hatua hiyo, huku wachambuzi wakitarajia mjadala zaidi wa kidiplomasia katika siku zijazo.

Leave a Comment