
Mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Iran na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2023, Narges Mohammadi, amehamishwa kutoka gerezani na kupelekwa hospitalini baada ya afya yake kudaiwa kuzorota kwa kasi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka taasisi yake, Mohammadi alipoteza fahamu mara mbili na kupata mshtuko mkali wa moyo akiwa gerezani, hali iliyosababisha madaktari wa gereza kuona kuwa hawezi kuendelea kupatiwa matibabu ndani ya kituo hicho.

Taarifa hiyo imesema kuwa uhamisho wake ulifanyika baada ya madaktari wa gereza kubaini kuwa hali yake haiwezi kudhibitiwa bila huduma maalum za kitaalamu mjini Tehran.
Awali, Mohammadi aliripotiwa kuzimia mara mbili katika gereza la Zanjan, kaskazini-magharibi mwa Iran, hali iliyozua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wanaharakati wa haki za binadamu.
Kwa mujibu wa mawakili wake, Mohammadi alishukiwa kupata mshtuko wa moyo mwishoni mwa Machi mwaka huu. Walipomtembelea siku chache baadaye, alionekana dhaifu, amepungua uzito, na akihitaji msaada wa muuguzi kutembea.
