
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ametoa onyo kali kwa watendaji wa sekta ya ardhi nchini, akiwataka kuacha mara moja tabia ya kuchochea na kusababisha migogoro ya ardhi inayojirudia mara kwa mara, akisema Serikali imechoshwa na malalamiko yasiyoisha kutoka kwa wananchi.
Akizungumza leo Mei 2, 2026, alipokutana na wananchi wa Idofi, Wilaya ya Makambako mkoani Njombe, Dk Nchemba amesisitiza kuwa haiwezekani kwa mtu kununua ardhi kihalali, kukamilisha taratibu zote na kupewa hati, kisha baadaye ardhi hiyo kuuzwa tena kwa mtu mwingine bila idhini ya mmiliki halali.

Ameeleza kuwa vitendo hivyo vinapaswa kukomeshwa mara moja na watendaji kuhakikisha wanazingatia sheria na haki za wananchi katika utoaji na usimamizi wa ardhi.
“Naelekeza yule mwingine aliyetoa fedha atafutiwe kiwanja kingine. Huyu mwenye hati halali na aliyelipia aendelee na shughuli zake. Haya ni mambo ya kipuuzi, hatuwezi kuendelea kuleta migogoro kila siku kwenye masuala ambayo hayapaswi kuwa na migogoro,” amesema Waziri Mkuu.
Kauli hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu mgogoro wa kiwanja uliowasilishwa mbele yake, ambapo amesisitiza kuwa serikali haitavumilia uzembe wala vitendo vinavyosababisha wananchi kukosa haki zao.
Serikali imeendelea kutoa wito kwa watendaji wa ardhi nchini kufanya kazi kwa weledi ili kupunguza migogoro inayozuia maendeleo na ustawi wa wananchi.
