
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Aprili 30, 2026, limemkamata mkazi wa Salasala, Kinondoni, Mocine Julius maarufu kama @mazidi, kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo kupitia mitandao ya kijamii zilizodai kuwa amenusurika kutekwa na watu wasiojulikana.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, uchunguzi wa awali umebaini kuwa taarifa hizo hazina ukweli na zililenga kuibua hofu na taharuki miongoni mwa wananchi.
Polisi wamesema mtuhumiwa huyo anashikiliwa kwa ajili ya mahojiano zaidi na hatua nyingine za kisheria zinaendelea kuchukuliwa kufuatia tukio hilo.
Jeshi la Polisi limeendelea kuwasihi wananchi kuwa waangalifu na kuhakikisha wanathibitisha ukweli wa taarifa kabla ya kuzisambaza mitandaoni, ili kuepuka kuchochea taharuki zisizo za lazima katika jamii.