×

Rais Samia Aeleza Mafanikio ya Ushirikiano na Rwanda Baada ya Mazungumzo na Kagame (Picha +Video)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Ziara ya Kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda Paul Kagame, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Mei, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Rwanda unaendelea kuimarika kwa kasi, huku thamani ya biashara kati ya mataifa hayo mawili ikifikia Shilingi bilioni 644 katika mwaka uliopita.

Rais Samia alitoa kauli hiyo Jumapili, Mei 3, 2026, jijini Dar es Salaam baada ya kufanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Paul Kagame, aliyeko nchini kwa ziara ya kikazi.

Rais wa Jamhuri ya Rwanda Paul Kagame akizungumza na Waandishi wa Habari kufuatia Ziara yake ya Kikazi Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Mei, 2026.

Mazungumzo hayo yalihusisha pia mawaziri na maofisa waandamizi kutoka pande zote mbili, yakilenga kuimarisha zaidi ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji kwa manufaa ya uchumi wa nchi hizo.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kuendeleza uhusiano huo wa kihistoria, akieleza kuwa una mchango mkubwa katika kufungua fursa za ajira, kukuza biashara na kuleta maendeleo ya pamoja kwa wananchi wa Tanzania na Rwanda.

Kwa mujibu wa Rais Samia, kuanzia Machi 1997 hadi Machi 2026, Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania imesajili jumla ya miradi 42 ya uwekezaji kutoka Rwanda yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 325.5.

Aliongeza kuwa miradi hiyo imechangia katika utoaji wa ajira kwa Watanzania 225, hatua aliyoitaja kuwa ni muhimu katika kukuza uchumi wa taifa na kuboresha maisha ya wananchi.

Ziara ya Rais Kagame nchini Tanzania inatarajiwa kuendelea kuimarisha zaidi mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi kati ya nchi hizi mbili jirani, huku matarajio yakiwa ni kuongeza kasi ya ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Kagame akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa Ziara ya Kikazi, tarehe 03 Mei, 2026
Rais Samia akipeana mkono na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda Paul Kagame.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo na Ujumbe wa Rwanda uliongozwa na Rais wa Nchi hiyo Mhe. Paul Kagame, tarehe 03 Mei, 2026.

  

Leave a Comment