
Kamati Kuu ya ACT Wazalendo imefanya tathmini ya kina ya Muhtasari wa Ripoti ya Tume ya Jaji Chande kuhusu mauaji ya raia Oktoba 2025 katika kikao cha dharura cha Chama hicho kilichofanyika Mei 03, 2026 katika Ukumbi wa Hakainde Hichilema uliopo katika Jengo la Maalim Seif, Makao Makuu ya Chama Dar es salaam.
Katika kikao hicho Kamati Kuu ya Chama hicho imefikia maazimio kadhaa ikiwemo kuendeleza msimamo weke wa kuikataa Tume ya Jaji Chande na Ripoti yake ikidai Tume hiyo iliundwa kwa ajili ya kuwasafisha (sanitize) wahusika wa mauwaji ya Oktoba 2025 badala ya kuwawajibisha.
Aidha ACT Wazalendo imetaja sababu za msingi za kuikataa Ripoti ya Jaji Chande ikieleza ripoti hiyo inawalinda wahusika wa mauaji kwa kukwepa uwajibikaji na inavisafisha vyombo vya ulinzi na usalama vilivyohusika badala ya kuviwajibisha huku ikitilia Shaka usahihi wa takwimu za Tume kuwa watu zaidi ya 518 waliuawa Oktoba 2025 ikihoji kwanini Tume imeshindwa kutumia takwimu hizo kutoa wito wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwajibika.
Sababu ya pili ya kamati hiyo kuikataa Ripoti ya Jaji Chande ni kwamba ripoti hiyo inawatia hatiani wananchi kwa kubadili malalamiko yao halali kuwa vurugu zilizopangwa. Kamati Kuu ya ACT Wazalendo imetaja sababu ya tatu ya kuikataa Ripoti ya Jaji Chande kuwa ni Tume imepuuza dhulma ya uchaguzi kuwa chanzo kikuu cha mgogoro na badala yake inahitimisha kuwa maandamano ya Oktoba 2025 yalipangwa na kufadhiliwa.
Kamati Kuu ya ACT Wazalendo imekitaja Chama hicho kama kielelezo cha wazi cha dhulma ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ikidai Mgombea wao wa Urais Ndg. Luhaga Joelson Mpina alizuiwa kugombea kwa sababu zisizokuwa na mantiki kisheria na Mahakama ya Rufaa haijashughulikia kesi yake hadi sasa.
