×

Trump Azindua “Project Freedom” Kusaidia Meli Hormuz, Iran Yapinga Vikali

Mwanasiasa mkuu wa Iran, Ebrahim Azizi, ameonya kuwa iwapo Marekani itaingilia mfumo mpya wa usimamizi wa baharini katika Mlango wa Bahari wa Strait of Hormuz, hatua hiyo itahesabiwa kama uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Azizi amesema eneo hilo nyeti halifai kuwa uwanja wa majibizano ya kisiasa, akisisitiza kuwa “Hakuna mtu atakayeamini simulizi za kulaumiana.” Ameongeza kuwa Ghuba ya Uajemi na Hormuz si maeneo ya kuendeshwa kwa matamshi ya uchochezi.

Kauli hiyo imekuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza mpango unaojulikana kama “Project Freedom”, unaolenga kusaidia usalama wa meli zinazopita katika mlango huo muhimu kuanzia Jumatatu, kwa mataifa yasiyohusika moja kwa moja katika mzozo kati ya Marekani, Israel na Iran.

Trump amesema operesheni hiyo itaanza rasmi Jumatatu, Mei 3, 2026, ikiwa na lengo la kuzipitisha salama meli na wafanyakazi wake waliokwama kwa zaidi ya miezi miwili kutokana na vizuizi vinavyohusishwa na Iran katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.

Katika ujumbe wake, Trump alisisitiza kuwa Marekani itaongoza meli hizo kuhakikisha zinapita kwa usalama, huku akionya kuwa jaribio lolote la kuzuia operesheni hiyo litakabiliwa na hatua kali.

Hatua hiyo imekuja wakati mvutano ukiendelea kuongezeka, ambapo Iran inadaiwa kuzuia usafirishaji wa mafuta na bidhaa kutoka Ghuba ya Uajemi, huku Marekani ikiweka vikwazo kwa meli zinazohusishwa na bandari za Iran.

Wakati huo huo, Iran imethibitisha kupokea majibu kutoka Marekani kuhusu pendekezo lake la amani lenye vipengele 14, likihusisha pia madai ya kuondolewa kwa vikwazo na kusitishwa kwa mapigano. Hata hivyo, Tehran imesema bado inalichambua pendekezo hilo.

Kwa upande wake, Trump ameonesha kutoridhishwa na mpango huo, akidokeza kuwa huenda usikubalike, wakati Iran ikisisitiza kuwa mazungumzo ya nyuklia hayawezi kuendelea hadi vita vitakapomalizika.

Leave a Comment