×

Mchumba wa Cristiano Ronaldo Atikisa Met Gala 2026 kwa Muonekano wa Kipekee

Mchumba wa nyota wa soka Cristiano Ronaldo, Georgina Rodriguez.

Mchumba wa nyota wa soka Cristiano Ronaldo, Georgina Rodriguez, ameonekana kung’ara kwenye hafla maarufu ya Met Gala 2026 iliyofanyika usiku wa kuamkia Mei 5, 2026 baada ya kuvaa vazi lililovutia hisia za wengi.

Georgina alijitokeza mjini New York akiwa amevalia gauni la rangi ya fedha lenye muundo wa kipekee, likiwa na sehemu ya juu iliyokuwa wazi zaidi na kupambwa kwa maua yaliyoshonwa, pamoja na mapambo ya vito na hereni kubwa zilizoongeza mvuto wake.

Akiwa kwenye zulia jekundu, aliweka pozi za kujiamini mbele ya kamera, akionyesha mwonekano uliowavutia mashabiki na watu maarufu waliokuwepo katika hafla hiyo ya mitindo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Georgina (32) aliwashukuru wale waliomsaidia kuandaa muonekano wake, akiandika:
“Kwa wale wasioonekana lakini wananiwezesha… asanteni kutoka moyoni. Timu yangu ni kama ndoto.”

Mashabiki wake zaidi ya milioni 70 walimiminika kwenye maoni wakimsifu, wakimuita “mrembo sana,” “mkamilifu,” na wengine wakimtaja kama “iconic” na “goddess.”

Georgina na Ronaldo walichumbiana rasmi mwezi Agosti 2025 baada ya kuwa pamoja kwa takriban miaka tisa, na wanatarajiwa kufunga ndoa baadaye mwaka huu. Kwa sasa, Ronaldo anaendelea kucheza soka katika klabu ya Al Nassr nchini Saudi Arabia.

Muonekano wa Georgina kwenye Met Gala umeendelea kuthibitisha nafasi yake kama mmoja wa watu wanaovutia zaidi kwenye ulimwengu wa mitindo na burudani.

Nyota wa soka Cristiano Ronaldo akiwa na mpenzi wake Georgina Rodriguez.

Leave a Comment