×

Exim Tanzania Yaimarisha Huduma za Afya Geita Kupitia Mpango wa Exim Cares

Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Abdallah Komba(kulia) akikabidhiwa moja ya vifaa vya hospitali vilivyotolewa na Afisa Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania Stanley Kafu (kushoto) kwa lengo la kurudisha kwa jamii. Hafla hii imefanyika kama moja ya huduma za Benki hiyo chini ya Mpango wa Exim Cares ambapo wanatoa misaada kwa sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na mazingira. Tukio hilo limefanyika tarehe 6 May 2026, Mkoani Geita.

Geita, Tanzania – 6 Mei 2026: Benki ya Exim Tanzania, kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) unaojulikana kama Exim Cares, imeunga mkono huduma za afya katika Hospitali ya Manispaa ya Geita, ikiwa ni hatua ya kuziba mapungufu muhimu katika huduma za afya ya uzazi na dharura, huku ikithibitisha tena dhamira yake ya kuboresha ustawi wa jamii inazozihudumia.

Msaada huu ni sehemu ya mpango wa kimkakati wa benki hiyo katika uwajibikaji kwa jamii, unaolenga maeneo muhimu yakiwemo afya, elimu, ubunifu, mazingira, na uwezeshaji wa kiuchumi. Kupitia nguzo hizi, benki imetekeleza miradi mbalimbali nchini, ikijumuisha programu za msaada wa tiba, kampeni za uchangiaji damu, ufadhili wa elimu na miradi ya uwezeshaji wa jamii yenye lengo la kuleta matokeo endelevu na ya maana.

Hatua hii ndani ya Geita umechochewa na uhitaji uliobainika ndani ya hospitali, ambapo upungufu wa vifaa muhimu vya tiba umekuwa ukizuia utoaji wa huduma kwa wakati na kwa ufanisi, hususani kwa wajawazito, watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda au wanoazaliwa na changamoto mbalimbali za kiafya. Kwa kuingilia kati katika maeneo haya muhimu, Benki ya Exim inalenga kuimarisha uwezo wa hospitali na kuboresha matokeo ya afya kwa jamii inayozunguka.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Mkuu wa Wilaya wa Geita, Mheshimiwa Hashim Abdallah Komba, aliipongeza Benki ya Exim na kuishukuru kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha afya ya watoto, hususan watoto njiti na wale wanaozaliwa na changamoto mbalimbali za kiafya. Pia alibainisha kuwa, licha ya benki hiyo bado kutokuwa na faida katika tawi lake jipya la Geita, imeonyesha moyo wa huruma na uwajibikaji kwa kuweka kipaumbele katika kusaidia jamii.

Aidha, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Stanley Kafu, alisema kuwa hatua hii inaonyesha mkakati wa makusudi na unaozingatia mahitaji halisi ya jamii.

“Kupitia Exim Cares, tunahakikisha tunalenga maeneo yanayogusa moja kwa moja maisha ya jamii inayotuzunguka. Hapa Geita, tulizungumza na wadau na kubaini mapungufu mahususi katika huduma za afya ya uzazi na watoto, na msaada huu unalenga kushughulikia kwa changamoto hizi kwa njia itakayosaidia jamii” alisema.

Mwakilishi wa Hospitali ya Manispaa ya Geita, Mganga Mfawidhi Dr. Thomas Mauru, aliipokea msaada huo kwa mikono miwili, akisema unakwenda sambamba na uhitaji wa haraka katika kuboresha huduma tajwa.
“Msaada huu utaongeza uwezo wetu wa kutoa huduma kwa wakati na kwa ufanisi, hususan kwa Watoto wanaozaliwa na changamoto mbalimbali za kiafya. Unachangia moja kwa moja kuboresha ubora wa huduma za afya tunazotoa kwa jamii yetu,” alisema.

Hatua hii inaakisi falsafa pana ya Benki ya Exim ya kuhakikisha ukuaji wake unaendana na maendeleo ya jamii inazozihudumia, na kuhakikisha kwamba kila benki inavyokua, inajibu mahitaji halisi ya wananchi.

Baada ya shughuli hii ya CSR, benki hiyo inatarajiwa pia kuzindua rasmi tawi lake jipya la Geita, hatua inayolenga kuimarisha zaidi uwepo wake katika mkoa huo na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa watu binafsi na biashara. Uzinduzi huo unatarajiwa kuongozwa na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde.

Kama sehemu ya mkakati wake wa muda mrefu, Benki ya Exim inaendelea kuwekeza katika suluhisho na ushirikiano unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha, kuchochea ukuaji wa biashara na kuimarisha mnyororo wa thamani, ikionesha nafasi yake si tu kama taasisi ya kifedha, bali pia mshirika wa maendeleo ya Tanzania.

Leave a Comment