
Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro linapenda kutoa ufafanuzi wa taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inayoeleza kuwa gari inayodhaniwa kuwa ni gari ya kubeba wagonjwa (Ambulance) kumtupa mtu mmoja mwanaume akiwa amefariki eneo la Mbwaruki Wilaya ya Moshi na kukimbia.
Uchunguzi wa awali unaeleza kuwa Mei 6, 2026 majira ya saa moja usiku mtu mmoja aitwaye Ismail Amani Mbowe (33), Mkazi wa Machame akiwa anaendesha pikipiki yenye namba za usajili MC 336FHV aina ya Sinoray akitokea uelekeo wa Himo kwenda uelekeo wa Moshi Mjini alipofika eneo la Uchira Karamsingi wakati akijaribu kulipita guta lililokuwa mbele yake alikwenda zaidi upande wa kulia na kugonga gari lenye namba za usajili T974EHQ/T947EJN aina ya Howo iliyokuwa inatoka Moshi mjini kuelekea Njiapanda na kupelekea kupata majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
Baada ya tukio hilo kutokea Wananchi walikusanyika na kutoa msaada wa awali kabla ya Polisi kufika eneo hilo, kwa kuomba msaada kwenye gari iliyotajwa kuwa ni gari ya wagonjwa kumkimbiza majeruhi huyo hospitali akiwa ameambatana na ndugu mmoja.
Wakiwa njiani inaelezwa kwamba gari hilo lilisimama na kumshusha majeruhi huyo na kuondoka kabla ya kumfikisha Hospitalini. Jitihada zilifanyika na majeruhi huyo alifikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi ambapo ilibainika amefariki dunia.
Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro linaendelea kufanya uchunguzi kubaini ukweli wa matukio yote mawili, ajali pamoja na gari iliyombeba majeruhi ambayo ilimshusha njiani kabla ya kumfikisha hospitali.
Aidha, Jeshi la Polisi linawasihi Wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia uchunguzi na kumpata dereva aliyefanya kitendo hicho.
