×

Iran na Marekani Zarushiana Makombora Hormuz, Trump Afunguka Mapya – Video

Rais wa Marekani, Donald Trump.

Rais wa Marekani, Donald Trump leo Mei 8, 2026 amesema kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran bado yapo imara licha ya kutokea kwa mapigano mapya katika eneo la Strait of Hormuz.

Jeshi la Marekani lilidai kuwa Iran ilishambulia meli zake tatu za kivita kwa kutumia makombora, droni pamoja na boti ndogo. Trump alisema Iran imejaribu kucheza na Marekani lakini akaonya kuwa Marekani iko tayari kujibu kwa nguvu zaidi endapo makubaliano hayatatekelezwa.

Kwa upande wake, Iran ilidai kuwa Marekani ndiyo iliyoanzisha mashambulizi baada ya kulenga meli ya mafuta ya Iran pamoja na maeneo ya pwani karibu na Bandar Khamir, Sirik na Kisiwa cha Qeshm. Jeshi la Iran lilisema lilijibu mashambulizi hayo kwa kulenga meli za kijeshi za Marekani.

Mvutano huo umeongezeka ikiwa ni siku moja tu tangu wizara ya mambo ya nje ya Iran kusema kuwa ilikuwa ikifikiria pendekezo la Marekani la kumaliza vita.

Wakati huo huo, wizara ya ulinzi ya Falme za Kiarabu (UAE) ilitangaza kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga ilikuwa ikikabiliana na mashambulizi ya makombora na droni yaliyodaiwa kutoka Iran.

Kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump alisema Marekani ilifanikiwa kuharibu boti kadhaa za Iran na kusisitiza kuwa Marekani haitasita kuchukua hatua kali zaidi iwapo Iran haitasaini makubaliano ya amani haraka.

Licha ya hali hiyo ya taharuki, mazungumzo ya kidiplomasia yanaendelea huku taarifa zikidai kuwa Marekani inaelekea kufikia makubaliano mapya ya hatua 14 yatakayoweka msingi wa mazungumzo zaidi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Leave a Comment