×

Waziri Dkt. Gwajima Asikitishwa Na Kukemea Mwenendo Wa ‘Mzee Malundo’ Mitandaoni – Video

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amekemea tabia ya mtu anayefahamika kwa jina la Mzee Malundo, ambaye hivi karibuni amesambaa katika mitandao ya kijamii kupitia video zenye viashiria vya mmomonyoko wa maadili baada ya kuonekana akijisifia kuwa katika mahusiano na mabinti wadogo maarufu kama “vitoto vya 2000.”

Kupitia vyombo vya habari, Dkt. Gwajima amekosoa vikali kauli na mwenendo huo, akieleza kuwa unakinzana na maadili, mila na desturi za Kitanzania. Aidha, amemtaka mhusika huyo kwenda kuzungumza na Baraza la Wazee kwa ajili ya kupewa nasaha na maelekezo sahihi ya maadili, akisisitiza kuwa wazee ndio walinzi na wasimamizi wa mila na desturi za jamii.

Mtu anayefahamika kwa jina la Mzee Malundo akiwa na binti wa 2000

Pia, Waziri Gwajima ametoa rai kwa vyombo vya habari na watumiaji wa mitandao ya kijamii kutokuwa sehemu ya kuchochea mmomonyoko wa maadili kwa kuwapa nafasi au umaarufu watu wenye maudhui yanayoharibu maadili ya Taifa.

“Sijui nisemeje huyu Mzee Malundo, huo ni ujinga kama ujinga mwingine. Haiwezekani mtu wa makamo kama wewe na kimo chako unatoka unaongea mambo kama hayo. Uliyafanya huko chumbani, unayaletaje kwenye umma?” amesema Dkt. Gwajima.

Leave a Comment