
Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer anakabiliwa na presha kubwa kutoka kwa wabunge wa Labour Party baada ya zaidi ya wabunge 20 wa chama hicho kumtaka aweke wazi ratiba ya kujiuzulu kufuatia matokeo mabaya ya uchaguzi wa mitaa nchini United Kingdom.
Starmer amesema anachukua jukumu la matokeo hayo huku akikiri kuwa wananchi wengi hawaamini kuwa Serikali yake inatekeleza vya kutosha kukabiliana na changamoto zinazowakabili. Hata hivyo, ameahidi kuendelea kujenga taifa lenye usawa na fursa kwa wote.
Katika uchaguzi huo, Reform UK kimeibuka na ushindi mkubwa nchini Uingereza baada ya kupata zaidi ya madiwani 1,400, huku Green Party nayo ikifanya vizuri kwa kuongeza madiwani 370 pamoja na kushinda nafasi mbili za umeya jijini London.
Kwa upande wa Liberal Democrats, chama hicho kilipata ongezeko la madiwani kwa mwaka wa nane mfululizo, ingawa mafanikio yake yalikuwa ya wastani ikilinganishwa na vyama vingine.
Matokeo hayo yamekuwa magumu zaidi kwa vyama vikubwa vya jadi, ambapo Conservative Party imepoteza zaidi ya viti 550 huku Labour ikipoteza karibu viti 1,400.
Kupitia Gazeti la The Guardian, Starmer amesema amefanya makosa lakini kusisitiza kuwa suluhisho si kuelekea zaidi kushoto au kulia kisiasa.
“Tunapaswa kujenga harakati pana za kisiasa, kusimamia maadili yetu kwa uthabiti, kuwa jasiri katika maono yetu na kushughulikia mahitaji ya wananchi huku tukileta umoja badala ya mgawanyiko,” amesema Starmer.