
Klabu ya Simba imeendelea kuthibitisha ubora wake katika soka la ndani na kimataifa baada ya kutwaa tuzo ya Klabu Bora ya Wanaume wa Mwaka katika Tuzo za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) 2025.
Tuzo hizo zimefanyika Mei 9, 2026 katika Ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam, zikihusisha wadau mbalimbali wa michezo nchini waliokusanyika kushuhudia na kutambua mafanikio ya wanamichezo, makocha, waamuzi pamoja na taasisi za michezo zilizofanya vizuri kwa mwaka 2025.
Tuzo ya Simba SC ilikabidhiwa na Gerson Msigwa ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, huku ikipokewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Zubeda Sakuru.
Katika tuzo za wanamichezo binafsi, mwanariadha nyota Alphonce Simbu ametwaa tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Kiume wa Mwaka kutokana na mafanikio yake katika mashindano ya kimataifa, huku Stumai Abdallah wa JKT Queens na Timu ya Taifa ya Wanawake akishinda tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Kike wa Mwaka.
Kwa upande wa vijana, Raymond Francis ametangazwa kuwa Mwanamichezo Bora Kijana wa Kiume, wakati Rose Kataboy akitwaa tuzo ya Mwanamichezo Bora Kijana wa Kike baada ya kuonyesha kiwango bora katika michezo yao kwa mwaka mzima wa 2025.
Aidha, tuzo nyingine zilizotolewa ni pamoja na Kocha Bora wa Kiume aliyekwenda kwa Anthony Mwingereza, Kocha Bora wa Kike aliyeshindwa na Esther Chabruma, huku Shabani Mahobonya akitwaa tuzo ya Mwamuzi Bora wa Kiume na Dariso Mwidadi kushinda tuzo ya Mwamuzi Bora wa Kike.
Katika upande wa habari za michezo, waandishi Fatma Chikawe na Khalid Msabaha walitunukiwa tuzo maalum kwa mchango wao katika tasnia ya habari za michezo nchini.
Tuzo za BMT zimeendelea kuwa chachu ya kuhamasisha ushindani, ubora na maendeleo ya michezo nchini Tanzania kwa kutambua mchango wa wadau mbalimbali waliofanya vizuri kila mwaka.