
Rais wa Marekani, Donald Trump, ameonyesha kutoridhishwa na majibu ya mwisho ya Iran kuhusu pendekezo la makubaliano ya kusitisha vita vinavyoendelea kati ya mataifa hayo.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye Truth Social siku ya Jumapili, Trump alisema majibu yaliyotolewa na Iran hayakubaliki kabisa.
“Nilisoma majibu kutoka kwa wanaojiita wawakilishi wa Iran. Siyapendi HAYAKUBALIKI KABISA!” aliandika Trump.
Kauli hiyo imekuja baada ya vyombo vya habari vya serikali ya Iran kuripoti kuwa Tehran tayari imewasilisha majibu yake kwa maandishi ya mapendekezo yaliyotolewa na Marekani kuhusu namna ya kumaliza vita hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Iran ilituma majibu hayo kupitia wapatanishi kutoka Pakistan.
Katika mahojiano yake na kipindi cha “Full Measure,” Trump pia alizungumzia operesheni za kijeshi za Marekani dhidi ya Iran, akisema taifa hilo bado lina uwezo wa kuendelea kushambulia malengo mengine ikiwa itahitajika.
Trump alidai kuwa Marekani tayari imefanikiwa kutekeleza takribani asilimia 70 ya malengo yake ya kijeshi dhidi ya Iran, huku akisisitiza kuwa uwezo wa nyuklia wa Iran umeathirika kwa kiwango kikubwa.
Aidha, rais huyo alisema Marekani inaendelea kufuatilia kwa karibu hifadhi ya uranium iliyorutubishwa ya Iran na kuonya kuwa hatua yoyote ya kujaribu kuisogeza inaweza kujibiwa kwa nguvu za kijeshi.
Pamoja na kauli zake kali, Trump hakuthibitisha rasmi kumalizika kwa mapigano, jambo linaloonyesha kuwa hali ya mvutano kati ya Marekani na Iran bado ipo katika kiwango cha juu.