×

Trump Atembelea China Baada ya Miaka 9, Aandika Historia Mpya – Picha

Rais wa Marekani, Donald Trump, amewasili mjini Beijing nchini China kwa ziara ya kihistoria ya siku mbili inayotarajiwa kufanyika Mei 14 hadi 15, katika hatua inayoonekana kuwa na umuhimu mkubwa katika siasa na uchumi wa kimataifa.

Ziara hiyo ni ya kwanza kwa rais wa Marekani aliye madarakani kutembelea China tangu mwaka 2017, jambo linaloifanya kuwa safari ya aina yake baada ya miaka tisa ya ukimya wa ziara za ngazi ya juu kati ya mataifa hayo mawili.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu ya Marekani (White House), Trump ameambatana na ujumbe mkubwa wa viongozi wa sekta binafsi, wakiwemo wakurugenzi wakuu wa kampuni kubwa kama Tesla, Elon Musk, pamoja na Apple, Tim Cook.

Mazungumzo ya ziara hiyo yanatarajiwa kulenga zaidi masuala ya biashara, uchumi wa dunia, teknolojia na ushirikiano wa kimkakati kati ya Marekani na China. Viongozi wa pande zote mbili wanatarajiwa pia kujadili changamoto za ushindani wa kiuchumi unaozidi kuongezeka kati ya mataifa hayo makubwa duniani.

Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanasema ziara hiyo inaweza kufungua ukurasa mpya wa mahusiano kati ya Washington na Beijing, au kuongeza misuguano iliyokuwepo tayari, kutegemea matokeo ya mazungumzo hayo.

Hata hivyo, macho ya dunia kwa sasa yako Beijing, yakisubiri kuona kama mkutano huo wa kihistoria utaleta mabadiliko chanya katika diplomasia ya mataifa makubwa duniani.

Leave a Comment