×

Serikali Yaipongeza SBL Kwa Kuwezesha Wakulima na Wenye Ulemavu

Dodoma, Tanzania – 17 Mei 2026: Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) imefanya kikao cha kimkakati na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu,  Prof. Palamagamba J.A. Kabudi (Mb), kujadili namna Serikali na sekta binafsi zinavyoweza kushirikiana katika kuharakisha mageuzi ya kijamii na kiuchumi pamoja na utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.

Mazungumzo hayo ya SBL yaliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Dkt. Obinna Anyalebechi, akiwa ameambatana na wajumbe wa timu ya uongozi wa juu wa kampuni.

Katika kikao hicho, SBL ilieleza dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono vipaumbele vya maendeleo ya taifa kupitia uwekezaji katika uzalishaji wa ndani, kuimarisha mnyororo wa thamani wa kilimo, kuongeza ajira, kuwawezesha vijana pamoja na kukuza uchumi endelevu. Mazungumzo hayo yalijikita katika mchango wa sekta binafsi katika kukuza ushiriki jumuishi wa kiuchumi, kuimarisha mnyororo wa ugavi wa ndani, na kusaidia utekelezaji wa vipaumbele vya taifa kupitia biashara zinazowajibika.

SBL inaendesha viwanda vyake katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Moshi, huku ikitoa ajira rasmi kwa Watanzania 800. Lakini pia kampuni hiyo imetoa ajira zisizo rasmi kwa zaidi ya wananchi 140,000 kupitia mnyororo wake mpana wa thamani unaojumuisha wasambazaji, wasafirishaji, wafanyabiashara wa rejareja, sekta ya ukarimu pamoja na wakulima.

Mwaka 2024, SBL ilinunua tani takribani 20,000 za nafaka kutoka ndani ya nchi, sawa na asilimia 80 ya malighafi zinazotumika katika uzalishaji wake. Kupitia ununuzi wa shayiri, mahindi na mtama kutoka kwa wakulima wa Tanzania, kampuni hiyo huchangia zaidi ya shilingi bilioni 12 kila mwaka katika mnyororo wa thamani wa kilimo nchini, hatua inayosaidia kukuza uchumi wa vijijini na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

SBL pia ilieleza maendeleo ya programu yake ya ununuzi jumuishi inayowawezesha zaidi ya wakulima 200 wenye ulemavu katika mkoa wa Singida kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Sightsavers, kupitia kilimo cha mtama. Kupitia programu ya Kilimo Viwanda, kampuni hiyo pia inawekeza katika kizazi kijacho cha wataalamu watakaosaidia maendeleo ya sekta ya kilimo viwanda nchini. Programu hiyo hutoa ufadhili wa masomo pamoja na mafunzo kwa vitendo kwa vijana wanaosomea masuala ya kilimo na biashara ya kilimo, ambapo zaidi ya wanafunzi 300 wamenufaika tangu kuanzishwa kwake.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Dkt. Obinna Anyalebechi alisema: “Kadri Tanzania inavyoendelea kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050, sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kusaidia ukuaji jumuishi wa uchumi, ujenzi wa ajira na uwekezaji endelevu. Kampuni ya Bia ya Serengeti itaendelea kujitoa katika kuchangia safari ya maendeleo ya Tanzania kupitia uzalishaji wa ndani, kuongeza thamani ya bidhaa pamoja na kujenga ushirikiano imara unaozalisha fursa za muda mrefu kwa Watanzania katika mnyororo wetu wa thamani.”

Kwa upande wake, Prof. Kabudi aliipongeza SBL kwa kuendelea kuwekeza nchini na kwa mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuimarisha ushiriki wa wazawa kwenye uchumi na kufanikisha agenda ya maendeleo ya muda mrefu ya taifa.

Kikao hicho kilihitimishwa kwa pande zote mbili kueleza dhamira ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuunga mkono maendeleo endelevu, ushiriki jumuishi wa kiuchumi pamoja na utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.

 

Leave a Comment