×

Hezbollah Yamshambulia Rais wa Lebanon Baada ya Ziara Yake Marekani

Kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran limemkosoa Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, likisema ziara yake nchini Marekani haikufanikisha malengo yaliyokusudiwa na imeonyesha serikali ya Lebanon “imejisalimisha kwa ushawishi wa mataifa ya kigeni.”

Katika taarifa iliyotolewa na wabunge wa Hezbollah, kundi hilo limesema ziara ya Aoun mjini Washington haikufanikiwa kupata ahadi kutoka Marekani ya kuishinikiza Israel kuondoa vikosi vyake katika maeneo ya Lebanon.

Aidha, Hezbollah imedai kuwa ziara hiyo haikusaidia kusitisha mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon, wala kuweka mazingira ya kurejea kwa usalama kwa wananchi waliokimbia makazi yao au kuanza kwa shughuli za ujenzi upya.

Rais wa Marekani Donald Trump alimkaribisha Joseph Aoun White House Jumanne, ambapo kiongozi huyo wa Lebanon alisisitiza umuhimu wa Israel kuondoa kikamilifu vikosi vyake kutoka ardhi ya Lebanon. Trump alisema Marekani “itaangalia suala hilo” alipoulizwa kama itaongeza shinikizo kwa Israel.

Hezbollah pia imekosoa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Lebanon na Israel yaliyoanza Aprili pamoja na makubaliano yanayoungwa mkono na Marekani yaliyosainiwa mwezi uliopita, ikisisitiza kuwa inapinga hatua hizo.

Wakati huo huo, Jeshi la Lebanon limeanza kupeleka wanajeshi katika eneo la Zawtar Al-Gharbiya kama sehemu ya utekelezaji wa makubaliano hayo. Chini ya mpango huo, jeshi linatarajiwa kulivua Hezbollah silaha katika baadhi ya maeneo huku vikosi vya Israel vikiondoka hatua kwa hatua.

Licha ya kupungua kwa kiwango cha mapigano katika wiki za hivi karibuni, Israel imeendelea kufanya mashambulizi ya mara kwa mara kusini mwa Lebanon. Siku ya Alhamisi, vyombo vya habari vya serikali ya Lebanon viliripoti mlipuko mkubwa karibu na mpaka na kujeruhiwa kwa mfanyakazi mmoja raia wa Syria kutokana na risasi zilizodaiwa kutoka kwa wanajeshi wa Israel.

Leave a Comment