
Serikali ya Pakistan imethibitisha kuwasilisha kwa Marekani mapendekezo mapya kutoka Iran yanayolenga kumaliza vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, huku mazungumzo ya kusaka amani yakielezwa kukwama na muda ukiendelea kuyoyoma.
Kwa mujibu wa chanzo kutoka Pakistan kilichonukuliwa na Reuters, mazungumzo hayo yanaendelea kupitia upatanishi wa Pakistan, lakini pande zote bado zina tofauti kubwa kuhusu masharti ya kusitisha kabisa mapigano.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei amethibitisha kuwa msimamo wa Tehran umefikishwa upande wa Marekani kupitia Pakistan, ingawa hakutoa maelezo zaidi kuhusu yaliyomo kwenye mapendekezo hayo.
Mapatano ya kusitisha mapigano kwa muda bado yapo baada ya wiki sita za vita zilizochochewa na mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Hata hivyo, Rais wa Marekani Donald Trump amesema makubaliano hayo yako kwenye hali tete.
Marekani inaitaka Iran kusitisha mpango wake wa nyuklia pamoja na kuondoa vizuizi katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, eneo muhimu linalopitisha sehemu kubwa ya mafuta duniani.
Kwa upande wake, Iran inataka kulipwa fidia ya uharibifu wa vita, kuondolewa kwa vizuizi dhidi ya bandari zake na kusimamishwa kwa mapigano katika maeneo yote ikiwemo Lebanon ambako Israel inapambana na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Tehran.
Trump pia ameonya kuwa muda wa Iran unazidi kuisha, akisema kupitia mtandao wake wa Truth Social kuwa Tehran inapaswa kuchukua hatua haraka kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Wakati huo huo, ripoti zinaeleza kuwa Trump anatarajiwa kukutana na washauri wake wa usalama wa taifa kujadili uwezekano wa kurejesha operesheni za kijeshi ikiwa mazungumzo yatashindikana.
Mvutano huo umeendelea kuathiri uchumi wa dunia huku mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika eneo la Ghuba yakisababisha kupanda kwa bei ya mafuta na kuongeza hofu ya mfumuko wa bei duniani.