×

Gawio Nmb Lapaa: Wanahisa Kula Neema ya Sh Bilioni 305

 

NMB Bank Plc imeweka rekodi mpya katika sekta ya benki nchini baada ya kupendekeza gawio la takribani Sh bilioni 305 kwa mwaka wa fedha wa 2025, likiwa ni sawa na Sh 610.15 kwa kila hisa. Gawio hilo linatajwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kutangazwa na benki hiyo na miongoni mwa malipo makubwa ya gawio katika historia ya sekta ya fedha nchini.

Kiwango hicho kinajumuisha gawio la kawaida la Sh 504.26 kwa kila hisa pamoja na gawio maalumu la Sh 105.89 kwa kila hisa, ambalo ni la kwanza katika historia ya NMB. Mapendekezo hayo yanatarajiwa kuwasilishwa kwa wanahisa katika Mkutano Mkuu wa 26 wa Mwaka utakaofanyika Juni 10, 2026, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, David Nchimbi, amesema kiwango hicho kinaifanya 2025 kuwa mwaka wa kihistoria kwa benki na sekta ya fedha nchini, huku, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu, Ruth Zaipuna, amesema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji thabiti wa Mpango Mkakati wa mwaka 2021 hadi 2025, uwekezaji katika teknolojia, maendeleo ya wafanyakazi na upanuzi wa huduma za fedha za kidijitali. Benki hiyo ilitangaza faida kabla ya kodi ya Sh trilioni 1.1, huku faida baada ya kodi ikifikia Sh bilioni 756 baada ya kukamilika kwa ukaguzi wa nje.

Ndani ya miaka mitano, jumla ya gawio la NMB imepanda kutoka Sh bilioni 48 mwaka 2020 hadi zaidi ya Sh bilioni 305 mwaka 2025, huku bei ya hisa ikiongezeka kutoka takribani Sh 2,340 hadi Sh 13,130. Hatua hiyo imeendelea kuimarisha nafasi ya NMB kama moja ya taasisi kubwa na zenye thamani kubwa zaidi za kifedha katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB Bank Plc, David Nchimbi (katikati), Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bank Plc, Ruth Zaipuna (kulia), na Mkurugenzi wa Uhusiano wa Wawekezaji, Uendelevu na Mawasiliano Innocent Yonazi (kushoto), wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu mapendekezo ya gawio la rekodi la Sh bilioni 305.08 kwa mwaka wa fedha wa 2025. Gawio hilo la Sh 610.15 kwa kila hisa linatarajiwa kuwasilishwa kwa wanahisa kwa ajili ya kuidhinishwa katika Mkutano Mkuu wa 26 wa Mwaka unaotarajiwa kufanyika Juni 10

Leave a Comment