×

TET Yataka Elimu Iendane na Mahitaji ya Dunia ya Sasa

 

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, amezitaka taasisi za elimu ya juu nchini kuhakikisha tafiti, ubunifu pamoja na matumizi ya teknolojia vinaelekezwa katika kutoa suluhisho la changamoto halisi zinazowakabili wananchi na kuchochea maendeleo ya taifa.

Dk. Komba alisema hayo wakati akifungua Maadhimisho ya Wiki ya 11 ya Utafiti na Ubunifu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kishiriki cha Elimu (DUCE), yaliyowakutanisha wanafunzi, wahadhiri, watafiti, wabunifu pamoja na wadau mbalimbali wa elimu na maendeleo.

Aidha, alieleza utayari wake wa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kishiriki cha Elimu (DUCE), Taasisi ya Global Education Link (GEL) pamoja na wadau wengine wa elimu nchini katika kuimarisha mwongozo wa taaluma kwa wanafunzi na walimu ili kuwaandaa vijana kuendana na mahitaji ya dunia ya sasa na ya baadaye.

Utayari huo umeelezwa na Dkt. Komba wakati alipotembelea banda la Global Education Link katika maadhimisho hayo, ambapo alisema changamoto ya mwongozo wa taaluma imekuwa kubwa nchini huku akisisitiza kuwa maandalizi ya mwanafunzi kuhusu mustakabali wake yanapaswa kuanza mapema tangu akiwa shule ya msingi.

Alisema maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana bila uwekezaji mkubwa katika elimu, tafiti, ubunifu, teknolojia na ushirikishwaji wa jamii, huku akisisitiza kuwa elimu bora haipaswi kuishia darasani pekee bali iwe nyenzo ya kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.

“Tafiti na ubunifu vinapaswa kuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa jamii. Tusifanye tafiti ambazo zinaishia kwenye makabati, bali tafiti zinazotoa majibu ya changamoto za wananchi,” alisema Dkt. Komba.

Alisema kuwa katika dunia ya sasa matumizi ya teknolojia na mifumo ya kidijitali ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa kazi, kuboresha huduma kwa jamii pamoja na kuharakisha maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, uchumi, mazingira, usafiri na afya.

Dkt. Komba alisema pia kuna umuhimu mkubwa wa kuwajengea uwezo walimu waliopo mashuleni ili wawe sehemu ya mfumo wa kuwaelekeza wanafunzi katika uchaguzi sahihi wa taaluma.

“Tunapaswa kuhakikisha watoto wanaelewa mapema wanataka kufanya nini katika maisha yao. Akishafanya maamuzi yasiyo sahihi katika hatua za awali inaweza kuwa changamoto kubwa baadaye,” alisema.

Leave a Comment