
Heart Team Africa Foundation (HTAF) kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wamezindua rasmi kampeni ya kitaifa ijulikanayo kama “Kutoa Ni Moyo” yenye lengo la kuchangisha fedha na kuhamasisha jamii kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo nchini Tanzania.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika jijini Dar es Salaam Mei 25, 2026, ukilenga kuunganisha Watanzania kutoka makundi mbalimbali ili kusaidia watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo kupata matibabu na huduma muhimu za afya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge amesema zaidi ya watoto 16,000 huzaliwa kila mwaka nchini wakiwa na matatizo ya moyo huku takribani watoto 4,000 wakihitaji upasuaji wa haraka.
Amesema hali hiyo inahitaji mshikamano wa kitaifa ili kusaidia familia zinazoshindwa kumudu gharama za matibabu.
“Kupitia kampeni ya Kutoa Ni Moyo tunatoa wito kwa Watanzania wote, taasisi binafsi na serikali kuwa sehemu ya harakati hii ya kuokoa maisha ya watoto,” alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HTAF, Dkt. Naizihijwa Majani amesema kampeni hiyo imelenga siyo tu kuchangisha fedha bali pia kuongeza uelewa kuhusu afya ya moyo na umuhimu wa jamii kushiriki kusaidia watoto wenye changamoto hiyo.
“Kutoa Ni Moyo si kampeni ya kuchangisha fedha pekee, ni harakati ya kitaifa inayojengwa juu ya mshikamano, huruma na dhamira ya kuokoa maisha ya watoto,” alisema Dkt. Majani.
Kwa mujibu wa takwimu za afya duniani, magonjwa ya moyo husababisha vifo vya watu milioni 17.9 kila mwaka duniani, huku mtoto mmoja kati ya 100 akizaliwa akiwa na tatizo la moyo.Kampeni hiyo inalenga kukusanya shilingi bilioni 25 zitakazotumika kugharamia upasuaji, matibabu, uchunguzi wa mapema pamoja na elimu ya afya ya moyo kwa jamii.
Aidha, kampeni itatumia mifumo ya kidijitali kuwezesha Watanzania wa ndani na nje ya nchi kuchangia kwa urahisi na uwazi.
Katika hatua nyingine, waandaaji wa kampeni hiyo wameeleza kuwa juhudi za awali tayari zimefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 3.08 kupitia michango ya fedha taslimu na vifaa tiba kutoka kwa wadau mbalimbali.
JKCI ni taasisi maalum ya taifa inayotoa huduma za matibabu ya moyo nchini Tanzania huku HTAF ikiwa taasisi inayosaidia mapambano dhidi ya magonjwa ya moyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi.